Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, ameendelea kuonesha dhamira thabiti ya serikali katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wote, bila kujali uraia. Akiwa jijini Arusha katika Kampeni ya Mama Samia ya msaada wa kisheria, Waziri Ndumbaro amesimamia utatuzi wa mgogoro mkali uliodumu kwa zaidi ya miaka saba kati ya raia watatu wa Italia waliokuwa wakitishiana maisha kutokana na biashara yao ya pamoja.
Raia hao, waliokuwa wameanzisha kampuni lakini baadaye kuingia kwenye mgogoro mkubwa, wameeleza kushukuru kwa jinsi serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ilivyowasaidia kupata suluhu ndani ya saa moja tu, jambo ambalo walishindwa kwa miaka yote hiyo.
Mbali na kutatua mgogoro huo, Waziri Ndumbaro amesema kampeni hiyo imeonyesha wazi kiu kubwa ya wananchi kuelewa sheria na njia bora za utatuzi wa migogoro. Huku akisisitiza kuwa huduma hiyo si kwa Watanzania pekee bali kwa yeyote anayeishi nchini, ameahidi Wizara yake kuendelea kutoa elimu zaidi kuhusu masuala ya kisheria ili kupunguza mizozo inayoweza kuepukika.