Skip to main content

CHIFU THADEO: SERIKALI YA RAIS SAMIA INASIMAMIA HAKI KWA WOTE

Submitted by admin on 5 March 2025

Katika Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inayoendelea katika Uwanja wa TBA mkoani Arusha, wananchi wameendelea kufurahia jinsi migogoro yao inavyoshughulikiwa kwa haraka na kwa haki.

Akizungumza Jumatano Machi 05, 2025 katika shughuli hiyo, Chifu Anthony Thadeo (Chifu Kapufi III) ameelezea namna serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inavyothamini haki kwa wananchi wote bila ubaguzi.

Amesisitiza kuwa hatua ya Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro kutatua migogoro ya wananchi siku iliyopita na uwepo wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) katika kampeni hiyo ni ishara kuwa haki inatekelezwa kwa vitendo.  

Chifu Thadeo ameeleza pia kuhusu kisa cha mwananchi mmoja aliyeambatana naye ambaye madai yake ni kufungiwa barabara, ambapo cha kushangaza ni kwamba aliyefunga barabara hiyo ni mwanasheria.

"Tazama hali ilivyo, mtu tunayemtegemea kulinda haki ndiye anayewanyima wananchi haki yao ya msingi," amesema. Hata hivyo, amefurahishwa na hatua za haraka zilizochukuliwa na wasimamizi wa sheria waliopo katika kampeni hiyo kuhakikisha tatizo hilo linashughulikiwa.

#mslac #sisinitanzania #katibanasheria #ssh #ccm #kaziiendelee #matokeochanya #nchiyangukwanza #habari #hakikwawote