Skip to main content

JAPAN KUSHIRIKIANA NA WIZARA KUENDELEZA SEKTA YA SHERIA NCHINI

Submitted by admin on 8 January 2025

Image

Image

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro leo tarehe 8 Januari, 2025 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa alipomtembelea Mhe. Waziri katika Ofisi za Wizara Mtumba jijini Dodoma kwa lengo la kumuaga baada ya kumaliza muda wake nchini.

Katika mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara Bw. Eliakim Maswi, Naibu Katibu Mkuu Dkt.Franklin Rwezimula na baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara Viongozi hao walijadiliana ni kwa namna gani mahusiano baina ya nchi hizo  yamekuwa yakiimarika katika sekta mbalimbali za kimaendeleo.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba  na Sheria Mhe.Dkt. Damas Ndumbaro  amempongeza Mhe. Balozi kwa kazi kubwa aliyoifanya na amesema kuwa Tanzania inathamini ushirikiano uliopo kati ya nchi hizi hususani kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA) ambalo limekuwa likitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. 

Waziri Ndumbaro ameongezea kuwa yapo maeneo katika sekta ya Sheria ambayo Nchi ya Japan kwa kushirikiana na Tanzania wanaweza kubadilishana uzoefu ili kuweza kusaidia Wananchi hususani katika maeneo ya vijijini ikiwa ni pamoja na masuala ya upatikanaji Haki pamoja na utatuzi wa migogoro. 

Kwa upande wake Balozi  Misawa amesema kuwa wataendelea kudumisha uhusiano uliopo baina ya Tanzania na Japan hususani katika sekta ya Sheria kwa kuwajengea uwezo Wataalamu  na kubadilishana uzoefu katika masuala ya utatuzi wa migogoro na usuluhishi.