Skip to main content

MAAFISA MAENDELEO WA DAWATI LA MSAADA WA KISHERIA WATOA ELIMU KWA WANUFAIKA WA TASAF HANDENI

Submitted by admin on 3 January 2025

Handeni, Tanga – Maafisa Maendeleo kutoka Dawati la Msaada wa Kisheria katika Halmashauri ya Mji wa Handeni wameendesha zoezi la kutoa elimu ya msaada wa kisheria kwa wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF). 

Katika kikao hicho, wanufaika walielimishwa kuhusu haki zao za kisheria, umuhimu wa msaada wa kisheria, na namna ya kushughulikia changamoto zinazohusiana na ardhi, urithi, ndoa, na masuala mengine ya kijamii kwa njia ya kisheria. 

Wananchi walionyesha furaha yao kubwa waliposikia kwamba Dawati la Msaada wa Kisheria limeanzishwa kwa agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili kuhakikisha haki inapatikana kwa kila mmoja, hasa wale wa kipato cha chini. 

Mmoja wa wanufaika wa TASAF aliyehudhuria kikao hicho alisema, “Hatukuwa tunajua kwamba kuna huduma kama hii ya msaada wa kisheria. Tunaishukuru sana serikali yetu chini ya Rais Samia kwa kuanzisha dawati hili, ambalo linaonyesha kujali haki na ustawi wa wanyonge.”

Kwa upande wao, Maafisa Maendeleo walisisitiza kuwa dawati hilo litakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Handeni katika kutatua migogoro mbalimbali na kuhakikisha kuwa kila mmoja anapata haki zake bila gharama kubwa. 

Uanzishwaji wa dawati hili unalenga kuwajengea uwezo wananchi, hasa wale walio katika hali ngumu kiuchumi, ili waweze kufikia haki kwa urahisi. Hii ni sehemu ya juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha maendeleo yanakwenda sambamba na haki za kijamii na kiuchumi. 

Elimu hii imepokelewa kwa shukrani kubwa kutoka kwa wanufaika wa TASAF, ambao wameelezea matumaini yao ya kupata msaada wa kisheria kwa changamoto wanazokutana nazo kila siku. #MSLAC #MSLAC #Katibanasheria #SSH #CCM #KaziIendelee #Nchiyangukwanza #SisiniTanzania #matokeochanya @samia_suluhu_hassan @IkuluMawasiliano