Skip to main content

MAMA ALIYETATULIWA MGOGORO WA ARDHI (MSLAC) ATOA SHUKRANI KWA RAIS SAMIA

Submitted by admin on 4 January 2025

Mama mmoja aliyekuwa na mgogoro wa ardhi amefanikiwa kupata haki yake kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Legal Aid Campaign (MSLAC), iliyofanyika kwenye viwanja vya Mwembetogwa, mkoani Iringa. 

Wakati wa kampeni hiyo, mama huyo alifika na kueleza changamoto yake ya mgogoro wa ardhi mbele ya mawakili na wataalamu wa sheria waliokuwa wakitoa msaada wa kisheria kwa wananchi. Baada ya kusikilizwa kwa kina, alipewa msaada wa kisheria ambao umewezesha mgogoro wake kutatuliwa kwa mafanikio makubwa.  

Leo hii, mama huyo amepewa kiwanja na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, hatua ambayo imemaliza kabisa mgogoro huo uliokuwa ukimkosesha amani. Akiwa na furaha na shukrani kubwa, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuanzisha na kuendeleza kampeni hii ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa hali ya chini.  

“Kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya MSLAC, nimepata haki yangu bila gharama yoyote. Namshukuru sana Rais Samia kwa kutujali sisi wananchi wa hali ya chini. Huu ni ushahidi kwamba serikali yetu ipo kwa ajili ya watu wake,” alisema mama huyo kwa furaha.  

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) imeendelea kuwa mkombozi kwa wananchi wengi nchini, hususan wale wenye changamoto za kisheria ambazo walishindwa kuzitatua kutokana na ukosefu wa maarifa ya sheria au uwezo wa kifedha. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imejidhatiti kuhakikisha haki inapatikana kwa wote kwa kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi.  

Kampeni hii imeendelea kuwa mfano bora wa jinsi serikali inavyoshirikiana na wadau mbalimbali wa sheria kuwasaidia wananchi, huku ikionyesha dhamira ya dhati ya Rais Samia katika kuhakikisha maendeleo jumuishi na haki kwa wote.