Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, imetangaza kuwa asilimia 75 ya wananchi wa Zanzibar wanatarajiwa kufikiwa na huduma za msaada wa kisheria kupitia Kampeni ya Mama Samia, itakayozinduliwa rasmi tarehe 23 Aprili 2025 katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Waziri wa Nchi, Mhe. Dkt. Mwl. Haroun Ali Suleiman, amesema kampeni hiyo itaendelea pia katika Kusini Unguja Mei 3, 2025 na Kusini Pemba, huku huduma zikitolewa kwa siku tisa mfululizo, kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 12 jioni.
Wananchi watapatiwa msaada wa kisheria bure kuhusu masuala ya:
•Ardhi
•Ukatili wa kijinsia
•Haki za binadamu
•Ndoa na talaka
•Mirathi
•Jinai na madai
Kampeni hii ni mwendelezo wa juhudi za awamu ya kwanza iliyoanza Mei 2023, ambapo wananchi 1,246 walinufaika.
Wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kufuatilia fursa hii adimu ya kupata haki bila gharama, huku vyombo vya habari vikihimizwa kuelimisha jamii juu ya kampeni hii muhimu kwa ustawi wa haki Zanzibar.