RUKWA – Wananchi wa Mkoa wa Rukwa wamejitokeza kwa wingi kushiriki katika uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, wakionesha shukrani na pongezi kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea huduma hii muhimu inayolenga kuwapatia haki na uelewa wa masuala ya kisheria.
Katika uzinduzi huo, wananchi walieleza furaha yao kwa hatua ya serikali kusogeza huduma za msaada wa kisheria karibu na jamii, jambo ambalo linasaidia kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakumba wananchi, hususan wale wasioweza kumudu gharama za mawakili. Wengi walisisitiza kuwa msaada huu ni hatua kubwa katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wote, bila kujali hali ya kiuchumi.
Wakizungumza wakati wa hafla hiyo, viongozi wa kampeni walieleza kuwa msaada wa kisheria utatolewa kwa wananchi wote bila ubaguzi, huku elimu ya kisheria ikitolewa kwa lengo la kuwasaidia wananchi kujua haki zao, taratibu za kisheria, na namna bora ya kutatua migogoro kupitia njia za kisheria.
Wananchi waliohudhuria waliipongeza serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha upendo na kujali ustawi wa wananchi kwa kuanzisha kampeni hii, ambayo imekuwa mkombozi kwa wengi. Walisema kuwa msaada huu wa kisheria unawapa nafasi ya kusimama kidete katika kutetea haki zao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inaendelea kutekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini, ikiwa na dhamira ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki yake kwa wakati na kwa njia sahihi.
#MSLAC #KatibanaSheria #SSH #CCM #KaziIendelee #NchiyanguKwanza #SisiniTanzania #matokeochanya