Mwanza, Februari 2025 – Zoezi la utoaji wa msaada wa kisheria jijini Mwanza limeendelea kushuhudia mwitikio mkubwa wa wananchi wanaohitaji ushauri na mwongozo wa kisheria kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo ardhi, mirathi, ndoa, masuala ya jinai, ukatili wa kijinsia, na ajira.
Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Wakili wa Serikali, Edith Shekibele, amesema kuwa idadi kubwa ya wananchi wamejitokeza kupata msaada wa kisheria, jambo linalodhihirisha hitaji kubwa la elimu ya sheria katika jamii.
"Tumeona mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi wanaokuja kupata msaada wa kisheria. Wengi wao wanakabiliwa na changamoto za kisheria lakini hawana uelewa wa taratibu za kisheria au namna ya kupata msaada," amesema Shekibele.
Ameongeza kuwa lengo la utoaji wa msaada wa kisheria ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata haki zake bila kikwazo cha kukosa uelewa wa sheria au ukosefu wa rasilimali za kugharamia huduma za kisheria.
Katika zoezi hili, taasisi mbalimbali za kisheria, mashirika yasiyo ya kiserikali, pamoja na mawakili wa kujitolea wanashirikiana kuhakikisha kuwa wananchi wanapata msaada stahiki wa kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi.
Wananchi waliohudhuria wameeleza kuwa msaada wa kisheria wanaoupata ni wa manufaa makubwa, ukiwasaidia kuelewa haki na wajibu wao katika masuala yanayowahusu, huku wengi wakishukuru serikali na wadau kwa kuleta huduma hizi karibu nao.
Zoezi hili litaendelea katika maeneo mengine ya jiji la Mwanza, likiwa ni sehemu ya juhudi za serikali na wadau wa sheria katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki kwa usawa na bila ubaguzi. #sisinitanzania #katibanasheria #kaziiendelee #mslac #ccm #ssh #nchiyangukwanza #habari #mwanza