Katika hatua muhimu ya kurejesha haki kwa wananchi, Timu ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia wilayani Hai imemkabidhi rasmi Mzee Assery Mushi shamba lake lenye ukubwa wa hekari moja lililopo katika kitongoji cha Landi, kijiji cha Kikavu Chini, kata ya Weruweru, wilaya ya Hai, mkoa wa Kilimanjaro.
Mgogoro wa shamba hilo kati ya Mzee Assery Mushi na Bw. Jacob Ogalo ulikuwa umedumu kwa muda mrefu, lakini baada ya timu hiyo kusikiliza hoja za pande zote mbili na kujiridhisha na maamuzi ya Baraza la Ardhi la Wilaya, haki imetendeka. Makabidhiano hayo yalifanyika mbele ya uongozi wa kitongoji, kijiji, kata, pamoja na majirani wa eneo hilo, yakithibitisha dhamira ya kampeni hiyo ya kusimamia haki za wananchi.
Hatua hii inaonyesha jinsi mpango wa msaada wa kisheria unavyosaidia kutatua migogoro ya ardhi kwa haki na uwazi, huku ukileta matumaini kwa wananchi wengi wanaokumbana na changamoto kama hizi.