Skip to main content

NIMEIONA SERIKALI YANGU KWA MACHO YANGU – ASANTENI KWA KUSIKILIZA KILIO CHANGU NA KUNISAIDIA

Submitted by admin on 18 April 2025

Bukoba Vijijini, Kagera – Katika kile kinachoonekana kuwa ushindi mkubwa wa haki na mafanikio ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Bi. Adelina Katula mkazi wa Halmashauri ya Bukoba Vijijini hatimaye amepata haki yake ya kupita katika kiwanja cha nyumba yake, baada ya miaka kadhaa ya kuishi katika mazingira magumu bila barabara ya kupita kuelekea nyumbani kwake.

Adelina ambaye alieleza kwa uchungu mbele ya Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo mkoani Kagera, alifafanua namna alivyohangaika tangu mwaka 2012 aliponunua shamba na kujenga nyumba, hadi 2020 alipoanza kuishi humo na kukuta hana njia ya kupita kutokana na waliomuuzia kukataa kumpa barabara.

Baada ya kutoa kilio chake hadharani, Waziri Ndumbaro alichukua hatua za haraka kwa kumkabidhi kwa maafisa wa Msaada wa Kisheria na kuahidi kuwa angetembelea halmashauri hiyo Jumatano ya wiki hiyo kuona kama haki imetendeka.

Leo, taarifa rasmi kutoka Bukoba Vijijini zinasema kuwa mgogoro huo umemalizika salama kwa maelewano ya kisheria, ambapo Adelina amepewa njia ya wazi ya kupita kuelekea nyumbani kwake. Kesi hiyo imetatuliwa kwa njia ya usuluhishi na makubaliano ya kisheria yaliyosimamiwa na wataalamu wa msaada wa kisheria pamoja na viongozi wa halmashauri.

Adelina akizungumza kwa furaha baada ya kupata haki yake amesema:

"Nashukuru sana kwa msaada huu wa kisheria. Nimehangaika kwa muda mrefu, lakini leo najiona huru kama mwananchi wa Tanzania mwenye haki. Nimeiona serikali yangu kwa macho yangu – asanteni kwa kusikiliza kilio changu na kunisaidia. Mama Samia asanteni kwa kampeni hii ya msaada wa kisheria, imenipa maisha mapya.” Kwa upande wake, Dkt. Damas Ndumbaro ametuma salamu za pongezi kwa timu ya Msaada wa Kisheria kwa kushughulikia suala hilo kwa kasi na ufanisi mkubwa, na kusisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kusimama na wananchi katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki bila ubaguzi wala vizingiti.