Wizara ya Katiba na sheria nchini Tanzania imeandaa Rasimu ya sera ya Taifa ya Jinai na Mkakati wa utekelezaji wa sera hiyo ambayo kulingana na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro, Sera hiyo inatarajiwa kuidhinishwa na serikali katika mwaka ujao wa serikali 2025/26.
Leo Jumatano Aprili 30, 2025, Bungeni Mjini Dodoma, wakati wa uwasilishaji wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Ndumbaro ameliambia Bunge kuwa lengo la Sera hiyo ni kuhakikisha kuwa kunakuwepo na mfumo Jumuishi utakaokuwa unashughulikia masuala ya Haki jinai.
Katika hatua nyingine, Waziri Ndumbaro akieleza programu mbalimbali zilizotekelezwa na Wizara yake kwa mwaka 2024/25, amesema Wizara hiyo pia imetoa mafunzo ya elimu ya uraia na utawala bora kwa wajumbe wa Kamati za usalama za Mikoa na Wilaya, watendaji wa Kata, Menejimenti na wataalamu wa Halmashauri zipatazo 122 katika Mikoa 17 ya Tanzania bara.
Aidha akizungumzia mkakati wa ujenzi wa kizazi chenye uzalendo, maadili na uwajibikaji, Waziri Ndumbaro amesema kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI na wizara ya Elimu, waliandaa maudhui ya Katiba na Uraia kwa shule za msingi, sekondari na vyuo vya mafunzo ya ufundi kote Tanzania bara.