Waziri wa Katiba na sheria nchini Tanzania Dkt. Damas Ndumbaro ameeleza kuwa katika kipindi cha Julai mwaka 2023 hadi Aprili 2024, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliendesha mashauri ya madai 9,013, ikifanikiwa kushinda mashauri 750 sawa na asilimia 77.6% ya mashauri yaliyomalizika na hivyo kufanikiwa kuokoa Bilioni 51.02, kiasi ambacho serikali ingelipa ikiwa ingeshindwa kwenye mashauri hayo.
Waziri Ndumbaro amebainisha hayo wakati wa uwasilishaji wa Hotuna ya bajeti ya Wizara ya Katiba na sheria kwa mwaka 2025/26, leo Jumatano Bungeni Mjini Dodoma, akieleza pia kwamba katika kipindi hicho mashauri ya usuluhishi 209 yalishughulikiwa, 21 yakimalizika, kati yake serikali ikishinda 16 na hivyo kuokoa Bilioni 16.92 pamoja na Dola za Marekani Milioni 63.34.
Waziri Ndumbaro pia amebainisha kuwa kwa mwaka 2024, Wizara yake ilifanya mapitio ya sheria ya usuluhishi sura ya 15 na kanuni zake ili kuwezesha uanzishwaji na uendeshaji wa kituo cha usuluhishi wa migogoro Tanzania, akiamini kwamba uwepo wake ni muhimu kwa maendeleo ya biashara na uwekezaji kwani huonesha kutunza amani ya pande zinazovutana, kupunguza muda wa ufuatiliaji wa kesi mahakamani pamoja na kudhibiti hasa zinazoweza kujitokeza katika uwekezaji na biashara kati ya pande zinazovutana.