Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa vibali vya ajira kwa sekta ya Mahakama nchini, akishukuru kwa Vibali vya ajira 522 vilivyotolewa mwaka jana na vibali Vingine 1044 vilivyotolewa mwaka huu.
Mhe. Sagini amebainisha hayo Jioni ya Aprili 30, 2025 wakati wa kuhitimisha mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2025/26, akieleza kuwa wameendelea pia kushughulikia uchakavu wa miundombinu ya mahakama kutokana na uwepo wa mahakama za Mwanzo na Mahakama za wilaya zilizokuwa zimejengwa tangu enzi ya Mkoloni.
Aidha Naibu Waziri Sagini ameeleza kuwa Wizara imepokea ushauri wa wabunge walioshauri Wizara na sekta ya mahakama kuwekeza nguvu katika ujenzi wa Mahakama kwenye ngazi za Tarafa kwa dhumuni la kuhakikisha Tarafa zote zinakuwa na Mahakama kabla ya kuhamia ngazi ya Kata.
Mhe. Sagini pia ameeleza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea na uimarishaji wa Miundombinu ya Mahakama kuu na Mahakama Jumuishi ngazi za Mikoa, akieleza pia kuhusu Ujenzi wa mahakama ngazi ya wilaya unaoendelea kwasasa kwenye Wilaya 72 kwamba Wilaya za Ileje na Kiteto zitajumuishwa katika Mpango huo.