Skip to main content

Timu ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Yawafikia Wananchi wa Kitumbikwela, Lindi

Submitted by admin on 25 February 2025

Lindi, Tanzania – Wananchi wa mtaa wa Kitumbikwela, kata ya Kitumbikwela ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, wamepata fursa ya kupokea msaada wa kisheria kupitia Timu ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC). Hatua hii ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha haki inapatikana kwa wananchi wote, hususan wale wanaokosa uelewa wa masuala ya kisheria. 

Katika mkutano uliofanyika Kitumbikwela, wananchi walielimishwa kuhusu haki zao za kisheria katika masuala ya ardhi, mirathi, ndoa, kesi za jinai, ukatili wa kijinsia, ajira, na umuhimu wa kuandika wosia. Viongozi wa kampeni hii walisisitiza matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro, ikiwemo usuluhishi, maridhiano, na mazungumzo badala ya kupeleka kesi mahakamani.  

Image

Wananchi waliopata huduma hiyo walieleza kuridhishwa na elimu waliyopewa, wakisema kuwa imewasaidia kuelewa taratibu za kisheria ambazo awali walikuwa hawazifahamu. Aidha, walitoa pongezi kwa juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake kwa wakati na kwa gharama nafuu.

Timu ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inaendelea na kampeni yake katika maeneo mbalimbali nchini, ikilenga kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kuongeza uelewa wa masuala ya kisheria na kusaidia upatikanaji wa haki kwa wote.

#MSLAC #KatibanaSheria #SSH #CCM #KaziIendelee #NchiyanguKwanza #SisiniTanzania #matokeochanya