Wananchi wa Monduli Juu mkoani Arusha wameeleza kufurahishwa na ujio wa kampeni ya Kitaifa ya msaada wa kisheria kwenye Kata yao, wakisema wananchi wengi wamekuwa na uoga wa kwenda Mahakamani, Polisi na kwenye vyombo vingine vya maamuzi, hivyo ujio wa wanasheria wa Mama Samia kwenye maeneo yao umekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wengi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Emairete ndugu Mboyo kayai Laizer amesema msaada huo wa kisheria umesaidia akinamama na watu wengi wenye shida waliokwama kwa masuala mbalimbali kutokana na hofu na kuhofia gharama za uendeshaji wa kesi hasa katika kupata fedha za kuwalipa mawakili pamoja na uduni wa elimu za kisheria.
Kampeni ya kitaifa Msaada wa kisheria ya Mama Samia imezinduliwa Machi 28, 2025 Mkoani Arusha, ukiwa ni mkoa wa 23 kufikiwa na kampeni hiyo, ikitarajiwa kwenda kwenye Kata na Wilaya zote za Mkoa wa Arusha kwa siku kumi, Kampeni ambayo imeasisiwa, kuratibiwa na kufadhiliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa chini ya Wizara ya Katiba na sheria.