Monduli, 25 Februari 2025 – Maafisa wa Kisheria wa Samia Legal Aid Campaign (MSLAC) kwa kushirikiana na Afisa Elimu ya Msingi Wilaya ya Monduli na viongozi wengine, wamehudhuria mkutano wa dharura uliofanyika Makuyuni kufuatia tukio la ukatili dhidi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Makuyuni lililotokea siku ya jana.
Mkutano huo umeitishwa baada ya maafisa wa kisheria kufanya mazungumzo na watoto waliokumbwa na tukio hilo na kutoa elimu ya haki za watoto. Hata hivyo, ilionekana kuwa elimu hiyo pekee haitoshi, na hivyo walimu wa shule walikubaliana kuitisha mkutano wa dharura ili kuwahusisha pia wazazi na jamii kwa ujumla.
Mwitikio wa mkutano ulikuwa mkubwa, ambapo wazazi walijitokeza kwa wingi kulaani vikali vitendo vya kikatili dhidi ya watoto. Wazazi wamesisitiza kuwa taasisi zinazohusika na utoaji wa haki zinapaswa kutenda haki ili kuhakikisha wahusika wanawajibishwa na ukatili wa aina hii unakomeshwa katika jamii.
Katika mkutano huo, maafisa wa kisheria wamewapa wananchi elimu kuhusu ukatili wa kijinsia, haki za watoto, haki za binadamu, na haki za makundi mbalimbali katika jamii. Wananchi wameshauriwa kushirikiana na vyombo vya sheria kwa kutoa taarifa na ushahidi ili kusaidia kukamilika kwa upelelezi na kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.
Kwa pamoja, wazazi, walimu, na viongozi wa jamii wamesisitiza mshikamano katika kuhakikisha mazingira salama kwa watoto na kuhimiza malezi bora yanayozingatia usalama na ustawi wa watoto wote wa Makuyuni.
#MSLAC #KatibanaSheria #SSH #CCM #KaziIendelee #NchiyanguKwanza #SisiniTanzania #matokeochanya