Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Kabudi amesema kuwa serikali inatambua mchango mkubwa unaofanywa na Legal Services Facility katika kuwezesha upatikanaji wa Haki kupitia Huduma za Msaada wa Kisheria kwa kuwawezesha Wasaidizi wa Kisheria kufika katika maeneo ya pembezoni na kuwapatia mafunzo hatua iliyopelekea huduma za Msaada wa Kisheria kuongezeka.

Aidha kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Legal Service Facility Bi. Lulu Gw’anakilala amehaidi kuendelea kushirikiana na serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kuwezesha Wasaidizi wa Kisheria kushiriki katika utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kikamilifu ili kuhakikisha kampeni hiyo inakua mkombozi kwa wananchi wote hasa wasioweza kumudu huduma hizo.

Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kusimamia masuala ya upatikanaji wa Haki Nchini ikiwa ni pamoja na kuratibu na kusimamia Huduma za Msaada wa Kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Msaada wa Kisheria Sura ya 21 ya Mwaka 2017, ambapo imeendelea kutekeleza jukumu la kusimamia na kuratibu utoaji wa huduma za msaada wa Kisheria nchini kwa kuhakikisha kwamba Mashirika ya watoa huduma za Msaada wa Kisheria yanatoa huduma iliyo bora kwa wananchi hususani wasiokuwa na uwezo.