Wizara ya Katiba na Sheria kupitia kwa Waziri Dkt. Damas Ndumbaro imeomba kuidhinishiwa na Bunge la Tanzania Jumla ya Shilingi Bilioni mia sita themanini na saba, milioni mia sita tisini na nane laki nne na themanini na tisa elfu kwaajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo kwa mwaka ujao wa fedha 2025/26.
Waziri Ndumbaro wakati akiwasilisha Hotuba ua Bajeti ya Wizara ya Katiba na sheria ameeleza kuwa Vipaumbele katika mwaka huo wa fedha vitakuwa ni pamoja na kuimarisha huduma msaada wa kisheria kwa wenye uhitaji pamoja na kushughulikia masuala ya Kikatiba na kutoa elimu ya Katiba na uraia kwa wananchi.
Wizara hiyo pia kwa mwaka 2025/26 imepanga kutekeleza mapendekezo ya Tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha Taasisi za haki jinai, kubainisha na kutatua migogoro ya kisheria kwa wananchi, kuimarisha mifumo ya utoaji haki pamoja na kuendelea kuimarisha ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa katika masuala ya Haki jinai na Haki madai.
Wizara pia kulingana na Waziri Ndumbaro, imepanga kuwezesha matumizi ya kiswahili katika sekta ya sheria, kuimarisha tafiti na tathmini ya mapitio ya sheria, ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika sekta ya sheria, pamoja na kuwezesha ajira, uteuzi na kuimarisha nidhamu na maadili kwa watumishi wa mahakama sambamba na kuimairhs matumizi ya TEHAMA na uendelezaji wa Rasilimali watu ndani ya Wizara na Taasisi zake.