Skip to main content

"JITOKEZENI! PATA HUDUMA ZA BURE ZA MSAADA WA KISHERIA KWA HAKI YAKO" - BI ESTER MSAMBAZI

Submitted by admin on 10 December 2024

Mkurugenzi wa Mama Samia Legal Aid Campaign (MSLAC), Bi. Ester Msambazi, ametoa wito kwa wananchi wote wa Tanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki na kufaidika na huduma za msaada wa kisheria wakati wa kampeni inayotarajiwa kutekelezwa katika mikoa ya Iringa, Songwe, Mara, na Morogoro. Kampeni hii maalum itaanza tarehe 10 Desemba 2024 na itaendelea kwa siku 10 mfululizo kwa kila mkoa. 

Akizungumza kuhusu kampeni hiyo, Bi. Msambazi alisisitiza kuwa huduma hizi ni muhimu katika kuhakikisha haki za msingi za kila Mtanzania zinalindwa na kuheshimiwa, bila kujali hali ya kiuchumi au kijamii ya mtu. “Kampeni hii inalenga kuwafikia wananchi wanaokosa fursa za msaada wa kisheria kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na changamoto za kiuchumi na kijamii,” alieleza. 

Huduma zitakazotolewa ni pamoja na ushauri wa kisheria, msaada wa kutatua migogoro ya kifamilia, ardhi, mirathi, na masuala mengine ya haki za binadamu. Kampeni hii pia inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao za kisheria kupitia mafunzo ya jamii na usambazaji wa machapisho yenye maelezo ya kina. 

Bi. Msambazi aliongeza kuwa lengo kuu la kampeni hii ni kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa wote bila ubaguzi. “Tunatoa wito kwa wananchi wote, bila kujali hali zao, kujitokeza katika vituo vya msaada wa kisheria vitakavyokuwa vimeandaliwa katika mikoa hii,” alisema. 

Kampeni ya Mama Samia Legal Aid ni moja ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan za kuimarisha upatikanaji wa haki kwa Watanzania wote. Wananchi wanashauriwa kufuatilia taarifa zaidi kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari ili kujua ratiba na maeneo ya utoaji huduma.