Skip to main content

MGOGORO WA ASKARI ALIYEPATA AJALI WAPATA SULUHISHO MBELE YA WAZIRI NDUMBARO

Submitted by admin on 9 April 2025

Katika tukio la kihistoria lililojiri wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia mkoani Tanga, Askari Halima Mvula Komba aliibua hoja nzito mbele ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, akieleza changamoto zinazomkabili katika kufuatilia haki zake baada ya kupata ajali akiwa kazini.

Askari Halima, kwa ujasiri na uchungu mkubwa, aliweka wazi masaibu aliyoyapitia, ikiwemo ucheleweshwaji wa fidia, kutotambuliwa ipasavyo hali yake ya kiafya, pamoja na kunyimwa baadhi ya maslahi yake ya msingi. Kati ya madai yake makubwa, ni kutopokea fedha kutoka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), licha ya kujeruhiwa akiwa kazini na kuwa katika hali inayohitaji msaada maalum wa kisheria na kijamii.

Mhe. Ndumbaro, baada ya kumsikiliza kwa makini, alitoa maagizo ya haraka kwa wataalamu wa sheria waliokuwepo kuhakikisha kuwa suala hilo linashughulikiwa mara moja kwa mujibu wa sheria, ili haki itendeke kwa Askari huyo shujaa.

Tukio hili limebainisha umuhimu wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, ikionesha jinsi ilivyo chachu ya kusikiliza na kutatua kero halisi za wananchi, hasa wanaohitaji msaada wa kisheria ili kupata haki zao.