Dodoma, 25 Februari 2025 – Maafisa wa maendeleo dawati la msaada wa kisheria leo wamehudhuria ufunguzi wa Kliniki ya Ardhi inayofanyika katika ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, eneo la zamani la CDA, karibu na SIDO. Kliniki hii imepangwa kuhudumu kwa siku nne, kuanzia tarehe 25 hadi 28 Februari 2025, ikitoa huduma mbalimbali za ardhi kwa wananchi.
Huduma zinazotolewa katika kliniki hii ni pamoja na: - Masuala ya umiliki wa ardhi (hati na nyaraka nyingine) - Huduma za mipango miji - Huduma za upimaji wa ardhi - Huduma za uthamini wa ardhi - Huduma za vibali vya ujenzi - Huduma za maliasili - Ushughulikiaji wa migogoro ya ardhi
Ufunguzi wa kliniki hii umefanywa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Alhaj Jabir Shekimweli,
akiambatana na Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Uendelezaji Makao Makuu ya Jiji la Dodoma, Bw. Moses Seleki, na Afisa Utumishi wa Jiji, Bw. Francis Kilawe, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Jiji. Pia, hafla hiyo imehudhuriwa na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mkuu wa Wilaya, Alhaj Shekimweli, alisisitiza mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa ili kuboresha utoaji wa huduma katika kliniki hii. Aliagiza yafuatayo:
1. Tathmini ya Kliniki za Nyuma: Kufanyika kwa uchambuzi wa kliniki zilizopita ili kubaini changamoto na mafanikio, hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma za ardhi kwa wananchi.
2. Huduma Maalum kwa Makundi Maalum: Kuanzishwa kwa meza maalum za kuhudumia wazee, watu wenye mahitaji maalum kama wajawazito na wale walio na watoto wachanga, ili kuharakisha upatikanaji wa huduma kwao.
3. Upatikanaji wa Huduma Kidigitali: Mkuu wa Wilaya alimuagiza Mkurugenzi wa Jiji kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa njia ya mtandao zinafanya kazi ipasavyo kwa kufunga router ili kuwezesha upatikanaji wa WiFi. Hatua hii itawawezesha wananchi kujihudumia kwa msaada wa maafisa TEHAMA.
4. Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Kijumuiya: Timu zinazoshughulikia migogoro ya ardhi zinapaswa kwenda moja kwa moja katika maeneo husika (site) ili kushughulikia changamoto hizo kwa ufanisi zaidi. Pia, alishauri kubadilisha timu za awali na kupeleka timu mpya ili kuona changamoto zinazojirudia na kutoa mawazo mapya ya kutatua matatizo hayo.
5. Kipaumbele kwa Migogoro Mikubwa: Mkuu wa Wilaya alisisitiza kuwa migogoro ya muda mrefu inayohusisha idadi kubwa ya wananchi, kama ile ya Ndachi, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, na Industrial Area (Kizota), ipewe kipaumbele katika utatuzi wake.
Akihitimisha hotuba yake, Mkuu wa Wilaya aliwahimiza wananchi wote wenye changamoto za ardhi kufika katika kliniki hiyo wakiwa na nyaraka zao muhimu, maelezo sahihi au ushuhuda ili kurahisisha mchakato wa kupata suluhisho la matatizo yao.
Kliniki hii inatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi na kupunguza migogoro ya ardhi ndani ya Jiji la Dodoma. #MSLAC #KatibanaSheria #SSH #CCM #KaziIendelee #NchiyanguKwanza #SisiniTanzania #matokeochanya