Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ametoa maelekezo mahususi kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, kuhakikisha kuwa sheria za nchi zinasimamiwa ipasavyo na kuheshimiwa. Rais Samia alisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa sheria kwa haki na usawa ili kudumisha amani, utulivu, na maendeleo endelevu ya taifa.
"Serikali inajenga misingi imara ya utawala bora, na jukumu lako kama Waziri wa Katiba na Sheria ni kuhakikisha kuwa kila sheria inayopitishwa inatekelezwa kwa haki. Nenda kasimamie sheria, na hakikisha hakuna anayevunja haki za wengine kwa makusudi au kutokana na uzembe.
" Rais Samia pia alitilia mkazo suala la utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi wa kipato cha chini, akisisitiza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria inapaswa kushirikiana na taasisi nyingine za kisheria, ili kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wote bila ubaguzi.
Dkt. Ndumbaro, ambaye alihudhuria hafla hiyo ya Uwapisho wake , aliahidi kuyatekeleza maelekezo ya Rais kwa bidii, akibainisha kuwa wizara yake itajielekeza katika kuimarisha mfumo wa sheria kwa kuongeza uwazi, uwajibikaji, na kuharakisha usikilizwaji wa mashauri katika mahakama.
"Nimepokea maelekezo haya kwa moyo wa dhati, na ninaahidi kuyatekeleza kwa vitendo. Tutaongeza kasi ya usimamizi wa sheria ili kulinda haki za kila Mtanzania," alisema Waziri Ndumbaro.
Maelekezo haya yanakuja wakati serikali ya Awamu ya Sita ikiwa imejipambanua kama kinara wa mageuzi makubwa katika sekta ya sheria na haki za binadamu, huku ikiwa imefanikiwa katika kuboresha miundombinu ya mahakama, kupunguza mlundikano wa kesi, na kuimarisha utoaji wa huduma za msaada wa kisheria.
Wananchi wamepongeza hatua ya Rais Samia, wakieleza kuwa msisitizo wake katika kusimamia sheria unaimarisha imani ya wananchi kwa serikali na mfumo wa sheria nchini.