Skip to main content

"RAIS WETU ANAWAJALI WANYONGE" – MHE. FLORENT LAURENT KYOMBO AWAOMBA WANANCHI WAJITOKEZE.

Submitted by admin on 25 February 2025

Pwani, Tanzania – Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imezindua rasmi Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia mkoani Pwani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa urahisi na bila gharama.

Uzinduzi wa kampeni hiyo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wanasheria, na wananchi, ambapo Mbunge - Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma hii ya bure. Ameeleza kuwa kampeni hii inalenga kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake kwa mujibu wa sheria, bila kujali hali yake ya kiuchumi.

“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wote. Ninawasihi wananchi wa Pwani kutumia fursa hii ya msaada wa kisheria bure ili kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili,” amesema Mheshimiwa Kyombo.  

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inalenga kutoa elimu ya sheria kwa wananchi, kuwahamasisha juu ya haki zao, na kuwapatia ushauri wa kisheria kwa wale wenye migogoro au changamoto za kisheria. Huduma zinazotolewa zinajumuisha masuala ya ardhi, mirathi, ndoa, ajira, na masuala ya kijinsia. 

Wananchi wa mkoa wa Pwani wameonyesha mwitikio mkubwa kwa kampeni hii, wakieleza kuwa ni fursa muhimu kwao kuelewa haki zao na namna ya kuzilinda kisheria. Serikali inatarajia kwamba kampeni hii itasaidia kupunguza migogoro ya kisheria katika jamii na kuimarisha utawala wa sheria nchini.  

Kwa mujibu wa Wizara ya Katiba na Sheria, kampeni hii itaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinawafikia wananchi wengi zaidi. #sisinitanzania #katibanasheria #kaziiendelee #mslac #ssh #ccm #matokeochanya #nchiyangukwanza #habari #sisinitanzania