Serikali ya Tanzania imechukua hatua kali dhidi ya vitendo vya ukatili na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kwa kutoa maagizo maalum kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba washukiwa wote wa vitendo hivyo wanakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.
Mauaji ya albino yamekuwa ni tatizo sugu katika nchi nyingi za Afrika Mashariki, ikiwemo Tanzania. Watu wenye ulemavu wa ngozi wamekuwa wakilengwa kutokana na imani potofu na ushirikina, ambapo viungo vyao hutumiwa kwa ajili ya kufanya dawa za kienyeji zinazodaiwa kuleta utajiri na bahati.
Maagizo ya serikali yametolewa na Waziri mkuu Kasim Majaliwa, bungeni mjini Dodoma. Maagizo haya yanaonyesha nia ya dhati ya kumaliza kabisa vitendo hivi vya kikatili. Serikali imeagiza Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi katika maeneo yenye watu wengi wenye ulemavu wa ngozi, kufanya misako maalum na kuanzisha uchunguzi wa kina ili kubaini mtandao wa watu wanaohusika na vitendo hivyo.