Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof Palamagamba John Kabudi leo tarehe 04 Desemba, 2024 amekutana na kufanya kikao na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu Mhe. Jaji Imani Aboud aliyeambatana na ujumbe kutoka Mahakama hiyo iliyopo jijini Arusha.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Wizara Mtumba, jijini Dodoma viongozi hao wamejadili kuhusu nafasi ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu katika kusimamia na kulinda Haki za Binadamu na Watu wa Afrika.
Waziri Kabudi amesema yapo maeneo ambayo yanahitaji kuboreshwa zaidi katika Mahakama ili kuimarisha mahusiano mazuri yaliyopo ambapo pia wamejadili changamoto zinazoikabili sekta ya Mahakama ambapo wamekubaliana kuendeleza majadiliano kwa ajili ya kuzifanyia kazi changamoto hizo ili kuiwezesha Mahakama kutimiza majukumu yake ambayo imepewa chini ya Mkataba wa kuanzishwa kwa Mahakama hiyo.