Waziri wa Katiba na sheria Mhe. Dkt Damas Ndumbaro ameeleza kuwa Kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia imetekelezwa katika Mikoa,Wilaya, Kata na Vijiji vyote vya Mikoa 30 ya Tanzania ikitekelezwa chini ya Falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ambaye pia ndiye muasisi na muwezeshaji wa Kampeni hiyo.
Dkt. Ndumbaro amebainisha hayo leo Jumatatu Juni 16, 2025, wakati wa salamu zake mbele ya wananchi wa Mbagala Jijini Dar Es salaam, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa kisheria kwa Mkoa wa Dar Es Salaam, kampeni inayozinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ikiwa pia ni sehemu ya uzinduzi rasmi wa Kampeni hiyo kwa awamu ya pili, ikitarajiwa tena kuzunguka kwenye Mikoa yote.
"Tumehakikisha tunafanya usuluhishi na watu wanafanya maridhiano. Tumehakikisha tunawaelimisha watu wawe wastahimilivu pale wanapokutana na changamoto za kisheria. Tumehakikisha kutokana na changamoto tulizozipata na mafunzo tuliyoyapitia tunafanya mabadiliko na tunajenga upya mifumo yetu ya kisheria." Amebainisha Waziri Ndumbaro.
Akizungumzia malengo ya Kampeni hiyo, Waziri Ndumbaro amebainisha kuwa lengo lake limekuwa ni kutoa elimu na ufahamu wa kisheria kwa watanzania wote pamoja na kutoa msaada wa kisheria kwa kila Mtanzania mwenye uhitaji. Kampeni hiyo imeongozwa na kaulimbiu isemayo " msaada wa kisheria, kwa haki, amani, usawa na maendeleo."