Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema ni dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Dkt. Hussein Mwinyi wa Zanzibar, kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanapata haki zao za msingi kwa ustawi wa maendeleo yao na ya Taifa kwa ujumla.
Mhe. Majaliwa amebainisha hayo leo Jumatatu Juni 16, 2025 Mbagalaz Temeke Mkoani Dar Es Salaam, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Mkoani humo, wakati alipomuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi huo, ikiwa ni Mkoa wa mwisho kati ya 32 inayotekeleza kampeni hiyo kwa awamu ya kwanza nchini Tanzania.
Akitoa salamu za Rais Dkt. Samia anayeendelea na Ziara yake ya Kikazi Mkoani Simiyu, salamu za Rais Dkt. Mwinyi na Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango, Majaliwa amebainisha kuwa Viongozi hao pia wamedhamiria Watanzania wote kuzijua sheria za nchi ili kuwawezesha kujisimamia wenyewe panapotokea matukio yanayovunja haki za kibinadamu nchini Tanzania.
Waziri Mkuu Majaliwa anazindua kampeni hiyo Jijini Dar Es salaam akiashiria pia uzinduzi rasmi wa kampeni hiyo kwa awamu ya pili nchini, kampeni yenye lengo la kutoa elimu na ufahamu wa kisheria pamoja na msaada wa kisheria, Kampeni ambayo imeasisiwa na kufadhiliwa na Rais Samia.